SURA YA KWANZA
VIPI TUTAMFAHAMU MOLA WETU NA WAPI TUICHUKUE IMANI
YA DINI YETU?
Hili ni swali muhimu mno na jawabu sahihi la swali hili ndiyo
ufumbuzi wa matatizo mengi yaliyojitokeza katika umma wa kiislamu,
kwa sababu waislamu wengi hawajui vipi watamfahamu mola wao
muumba, na wapi wanatakiwa kuichukua dini yao !
Ama Ahlu Sunna wal Jama’a wao wanaitakidi kwamba:
Tutamjua mola wetu kwa vile alivyojielezea yeye mwenyewe katika
kitabu chake (Qur’an tukufu) na vile alivyotuelezea mjumbe wake
mtukufu katika mafundisho yake yaliyo sahihi.
Kwa kuyathibitisha yale yote ambayo Allah amejithibitishia mwenyewe
au ambayo ameyathibitisha Mtume wake -swalla llaahu alayhi
wasallam-, na kuzikanusha sifa ambazo Allah na Mtume wake
swalla llaahu alaihi wasallam wamezikanusha, bila ya kupotosha,
wala kupinga, wala kumfananisha yeye na chochote katika viumbe
vyake, pamoja na kufuta dhana ya kwamba kuyathibitisha yale
ambayo Allah amejisifia nayo kuwa ni kumfananisha yeye –Jalla
Jalaaluh- na viumbe vyake.
Na tunaichukua imani ya dini yetu kutoka kwenye Qur’an na Sunna
(mafundisho) sahihi ya Mtume wetu Muhammad -swalla llaahu
alayhi wasallam- pamoja na kuuzingatia ufahamu wa Salaf Swaalih
(wema waliotangulia) kama vile; Maswahaba na Taabi’ina
(wanafunzi wa Maswahaba) na maulamaa waliokuja baada yao.
Na hivi ndivyo tulivyoamrishwa na Qur’an kadhalika Sunna sahihi za
Mtume swalla llaahu alayhi wasallam.
Amesema Allah -azza wajalla-:
وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ آمِنُواْ آَمَا آمَنَ النَّاسُ قَالُواْ أَنُؤْمِنُ آَمَا آمَنَ السُّفَهَاء أَلا إِنَّهُمْ هُمُ السُّفَهَاء وَلَكِن لاَّ يَعْلَمُون}
“Na wanapoambiwa:aminini KAMA WALIVYOAMINI WATU wanasema;
Tuamini kama walivyoamini wapumbavu?...”.
Suratul-Baqarah aya ya 13.
Imepokewa kutoka kwa Ibnu Mas’oud na Ibn Abbaas kwamba
wamesema: “Watu waliokusudiwa hapa ni maswahaba”.
Tazama tafsiri al-Durrul-Manthuur juzuu ya 1 ukurasa 70-71.
Na maana ya aya hii ni kwamba makafiri na wanafiki walikuwa
wakiambiwa kwamba wamuamini Allah kama walivyoamini Maswahaba
wa Mtume Muhammad -swalla llaahu alayhi wasallam- wao kwa
sababu ya kiburi, na jeuri zao walikuwa wakiwatukana Maswahaba
kwa kuwaita wapumbavu, na hali ya kuwa wapumbavu ni wao !
Na amesema tena Allah:
فَإِنْ آمَنُواْ بِمِثْلِ مَا آمَنتُم بِهِ فَقَدِ اهْتَدَواْ وَّإِن تَوَلَّوْاْ فَإِنَّمَا هُمْ فِي شِقَاقٍ فَسَيَكْفِيكَهُمُ اللّهُ وَهُوَ السَّمِيعُ
الْعَلِيمُ البقرة 137
“Basi wakiamini KAMA MLIVYOAMINI NYINYI (maswahaba) basi
watakuwa wameongoka.Na wakikengeuka basi wao wamo katika
upinzani”.
Suratul Baqarah aya ya 137.
Katika aya hii Allah anawataka Ahlul-kitabi (Mayahudi na Wakristo)
wamuamini Allah kama walivyoamini Maswahaba na waislamu wote
kwa ujumla walio na imani kama ya Maswahaba, na kama wataasi
wakenda kinyume na Amri hiyo, basi wao watakuwa ni waasi na ni
wapinzani wa Allah.
Na amesema tena Allah:“Na anaye mpinga Mtume baada ya kumdhihirikia uwongofu na
AKAFUATA NJIA ISIYOKUWA YA WAUMINI,tutamuelekeza alikoelekea
mwenyewe,na tutamuingiza katika Jahannamu....”.
Surat An Nisaa aya ya 115.
Amesema Allah:
والسابقون الأولون من المهاجرين والأنصار والذين اتبعوهم بإحسان رضي الله عنهم ورضوا
عنه...الآية
“Na wale waliotangulia, wakwanza katika Muhajirina na Answaari,na
wale waliowafuata kwa wema, Allah ameridhika nao, na wao
wameridhika naye....”.
Suratut Tawba aya ya 100.
Kwa mujibu wa aya hizo zote tulizozitaja, tunatakiwa waislamu wote
kuamini kama walivyoamini maswahaba wa Mtume Muhammad -
swalla llaahu alayhi wasallam- pamoja na kuifuata njia waliyoipita.
Na kama imani zetu zitatofautiana na imani zao na njia yetu
ikitofautiana na njia yao, basi tutakuwa ndani ya mashaka makubwa
mno na upotevu uliowazi kama zilivyoeleza aya tulizozitaja.
Hivyo basi, tunapolizungumzia suala zima la kumuamini Allah –
Sub’haanahu Wata’alaa- ni lazima tujiulize maswali yafuatayo:
Je imani zetu zinaendana na mafundisho ya Qur’an na Sunna kama
walivyofahamu wema waliotangulia (Salaf Swalih)?
Je hivi tunavyoitakidi ndivyo walivyoitakidi hao Salafu Swalihi (wema
waliotangulia) au la?
Na kama jawabu likiwa la, basi tujue kwamba tumo ndani ya
upotevu kwa kuifuata njia isiyokuwa ya hao waumini wa mwanzo.
ومن يشاقق الرسول من بعد ما تبين له الهدى ويتبع غير سبيل المؤمنين نوله ما تولّى
ونصله جهنم.. الآية
Na bila shaka, wao wameifahamu vizuri Qur’an na walimfahamu
vizuri Mtume -swalla llaahu alayhi wasallam- kuliko walivyomfahamu
na wanavyomfahamu na watakavyofahamu watakaokuja baada yao,
ndiyo maana Allah akawasifia wao na wale walioifuata njia yao kwa
wema, na akawaahidi mambo mazuri.
Na wakati huo huo akawasema vibaya wale waliyoihalifu njia hiyo,
na kuwaandalia makazi mabaya motoni -Allah atuepushe na adhabu
zake-.
Hivyo basi, katika suala hili la kuonekana au kutokuonekana Allah
kwa macho huko akhera pia tunatakiwa pale tunapozitazama aya na
hadithi zinazo lizungumzia suala hili tuutangulize mbele ufahamu wa
hao wema waliotutangulia (Salafu Swalihi) katika imani, vipi wao
walizifahamu aya na hadithi hizo?
Na ilikuwaje imani yao juu ya suala hilo?
Je waliamini kwamba Allah ataonekena kwa macho huko akhera
kama wanavyo amini Ahli Sunna?
Au Allah hataonekana kwa macho huko akhera kama ilivyokuwa
itikadi ya makundi mengine kama vile: Jah’miyyah, Mu’tazila na
wajukuu zao kama vile Shia, Ibadhi na wengineo miongoni mwa
watu wa bid’a?
Inshaallah swali hili litajibiwa na kitabu chetu hiki, tafadhali fuatilia
kwa makini na insafu utagundua ukweli juu ya suala hili.
Huenda mtu akatatizika au akatatizwa kwa kuambiwa: vipi tufuate
njia ya hao waliotangulia (Maswahaba,Taabi’ina, na Maimamu
waliokuja baada yao) na hali yakuwa wao wenyewe wametofautiana
katika mambo mbalimbali?
Jawabu ni kwamba; tutashikamana na ufahamu wao katika mambo
ambayo wameafikiana, na yale waliyotofautiana sisi tutaichukua kauli
iliyoungwa mkono na maandiko sahihi, na wala haifai kuzusha kauli
ya tatu zaidi ya kauli zao mbili zilizo tofauti.
Ama mambo ambayo hayakuwepo katika wakati wao katika yale
ambayo yanafaa kutumia akili na rai, basi huo ndiyo uwanja wa
kuogelea maulamaa katika kufanya ijtihadi na kutumia rai zao kwa
mujibu wa kanuni na misingi ya kielimu.
Swali la kujiuliza ni; Je hao wema waliotangulia wametofautiana juu
ya suala la kumuona Allah kwa macho huko akhera?
Jawabu ni kwamba:
Maswahaba Hawakutofautiana katika suala hili, bali wote waliafikiana
kwamba watu wema watamuona mola wao kwa macho huko akhera
kama lilivyo thibitishwa suala hilo na Qur’an na Sunna sahihi za
Mtume –swalla llaahu alayhi wasallam-.
Na hakuna mtu yeyote aliyemuona, wala atakayemuona Allah kwa
macho yake hapa duniani, na hivyo ndivyo wanavyoamini na kuitakidi
Ah’lu Sunna Wal-jamaa.
Lakini tofauti imekuja katika jambo ambalo ni nje ya maudhui yetu
hii, jambo lenyewe ni: Je bwana Mtume –swalla llaahu alayhi
wasallam- alimuona Mola wake katika usiku aliokwenda mbinguni
(Miraji) ?
Jawabu ni kwamba, kuna kauli iliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas -
Allah amridhie- kwamba; bwana Mtume –swalla llaahu alayhi
wasallam- alimuona Mola wake katika usiku huo.
Wengi katika wanavyuoni wakayachukulia maneno yake hayo kwamba,
makusudio yake ni kuwa bwana Mtume alimuona Mola wake kwa
moyo wake, na wakategemea riwaya nyingine zilizopokewa kutoka
kwa huyo huyo Ibn Abbas.
Ama kuhusu suala la kumuona Allah usingizini hili pia si katika
maudhui ya kitabu hiki.
Comments
Post a Comment